
Je, nanii anastahili kuwa nahodha mpya wa Simba?
“Mara zote huwa nawaachia wachezaji wangu wamchague nahodha wao, sikupenda kilichofanyika msimu uliopita, msimu huu nitachagua nahodha mimi mwenyewe,” kauli ya kocha wa Manchester City, Pep Guardiola kabla ya msimu huu kuanza.
Linapofika suala la uteuzi wa nahodha wa timu huwa kuna vigezo vingi vya kuzingatia. Uongozi wa asili (leardership), uwezo wake wa kuwasiliana, uzoefu wake na nidhamu. Klabu ya Simba imeondokewa na manahodha wake wawili katika dirisha hili kuelekea msimu wa 2025/26.
Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyesajiliwa Yanga na Fabrice Ngoma aliyeondoka mwishoni mwa msimu.
Ngoma raia wa DR Congo alijiunga na kikosi cha Simba kutoka Al Hilal ya Sudan Julai mwaka 2023 kwa mkataba wa miaka miwili.
Inatajwa sababu ya Kocha Fadlu Davids, kumteua kuwa nahodha msaidizi wa Simba, Fabrice Ngoma ni nidhamu yake.
Kuelekea msimu wa mwaka 2025/26, Simba italazimika kuteua nahodha mpya. Vigezo vikiwa ni nidhamu, uzoefu, uwezo wa kuwasiliana na kuwa na uongozi wa asili.
Je, nani anastahili kuwa nahodha wa Simba?
Majina mawili yanatajwa kuwa manahodha wa klabu hiyo, Shomari Kapombe na Mzamiru Yassin. Kwa kigezo za uzoefu, hawa ni wachezaji waandamizi ndani klabu ya Simba.
Shomari Kapombe, amedumu Simba tangu mwaka 2017 aliporejea kwa mara ya pili akitokea Azam. Kapombe, aliichezea Simba kwa mara ya kwanza msimu wa mwaka 2011 hadi 2013 kabla kusajiliwa AS Cannes.
Kwa upande wa Mzamiru Yassin, alijiunga na Simba mwaka 2016 akitokea Mtibwa Sugar, tangu hapo amekua na nyakati nyingi nzuri Simba kabla ya kupoteza namba msimu uliopita kutokana na usajili wa Yusuf Kagoma.
Je, Mzamiru Yassin kuwa nahodha msaidizi wa Simba? Shomari Kapombe kuwa nahodha mkuu wa Simba? Siku ya Tamasha la Simba (Simba Day) atatangazwa nahodha mpya wa klabu hiyo.